Huu wimbo ulitoka rasmi wiki iliyopita. Kwa makusudi sikuuweka hewani. Nilikuwa na bado nina maana yangu. Ukiendelea kusoma bila shaka utanielewa.
Kila kizazi kina tabia au haki ya kudai kwamba muziki wao, wa enzi zao, ni bora kuliko wa kizazi kingine. Bila shaka hilo halikushangazi. Ulitegemea kizazi fulani kiseme kwamba chao kilikuwa au ni cha mbumbumbu wasio wabunifu wala wenye kuchangamsha akili zao na kutengeneza vitu vya nadra?! Sidhani….mwamba ngoma huvutia upande wake. Ni hulka ya binadamu.
Lakini historia ya binadamu inaonyesha kwamba mahali ambapo binadamu alifanya vyema zaidi ni pale aliposhirikiana na wenzake.Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Bila shaka kuna kila aina ya ukweli katika hili.
Kwenye sanaa ya muziki nchini Tanzania, miongoni mwa wasanii ambao wameamua kwa makusudi kuileta dhana hiyo kwa vitendo ni MwanaFA. Yeye(na nakubaliana naye kabisa) anaamini kwamba kila kizazi kina yake mazuri. Cha msingi ni kuendeleza yale mazuri na kuachana na yale ambayo hayana maana. Kuna muziki mzuri kutoka kizazi kile. Kuna muziki mzuri kutoka kizazi hiki.Kwanini tusichanganye tukapata kizuri zaidi? Ameeita kampeni yake Keeping The Good Music Alive.
Hicho ndicho alichokizangatia alipotoka na Yalaiti ikiwa ni maingiliano ya enzi zile za Sitti Binti Saad na sasa. Linah akaingia na kukoleza ya kale na mapya. Huu hapa sasa ni ujio wake katika wimbo Kama Zamani akiwa amewashirikisha The Kilimanjaro Band (Njenje) na Mandojo & Domokaya.
Sasa kwanini nimesubiri mpaka leo kuweka post hii? Ni hivi; naunga mkono harakati hizi za MwanaFa za Keeping The Good Music Alive. Niliona kwa sababu naunga mkono juhudi hizi, basi nisubiri kwanza kibao hicho kipatikane kwenye platforms mbalimbali za mtandaoni ambapo na wewe unaweza kuunga mkono jitihada zake kwa kuununua copy yako.Usikilize hapa chini…lakini kama unaamini kwamba muziki mzuri unahitaji maandalizi mengi na yenye kugharimu, basi tafadhali ungana nami katika juhudi za kuwasaidia wasanii wetu(akiwemo MwanaFA) kwa kununua kazi yake.
Naam unaweza kununua wimbo huu kwa kufuata Links hizi.Kumbuka ORIGINALS ARE MASTERPIECES.Let’s support our artists(especially those who makes good music). Nunua kupitia Links Zifuatazo;
KUNUNUA KUPITIA AMAZON BONYEZA HAPA