Quantcast
Channel: Bongo Fleva – Bongo Celebrity
Viewing all articles
Browse latest Browse all 180

Ray C Aingia Tena Rehab

$
0
0

Rehema Chalamila Ray C na matumizi ya madawa ya kulevya

Mara nyingi huwa natamani nisiandike kuhusu kuanguka kwa mtu. Sipendi. Lakini kama kwa kuandika kuhusu kuanguka kunaweza kusaidia aliyeanguka au mwingine ambaye asiposikia ataanguka,basi yatubidi.

Majuzi kwenye mitandao ya kijamii ilisambaa video inayomuonyesha mwanamuziki wa siku nyingi, Rehema Chalamila maarufu kama Ray C akiwa katika hali ya kusikitisha kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya.

Video hiyo ilimuonyesha akiwa anasaidiwa na Polisi. She was hallucinating. Inadaiwa alikuwa anataka kujidhuru mwenyewe. Ilisikitisha na kuliza wengi. Ray C ni miongoni mwa wanamuziki waliowahi kutamba na bila shaka ana kipaji. Hivi sasa kipaji kinaangamia kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya. Polisi wale waliokoa maisha yake. Wanastahili pongezi nyingi. Wameitenda kazi yao ya kulinda uhai na usalama wa raia. Wasingejitokeza pale, wakati ule,huenda leo tungekuwa tunaongea mengine.

Ray C goes to rehab

Habari njema ambazo zimepatikana ni kwamba Ray C amepelekwa Life And Hope Rehabilitation Centre (Sober House) iliyopo Bagamoyo kwa ajili ya kusaidiwa kuachana na matumizi ya madawa hayo. Kituo hicho ndicho ambacho hivi karibuni kilimsaidia mwanamuziki mwingine, Chizi Benz. Baada ya kutoka huko Chidi Benz ameonekana kuwa katika hali nzuri kiafya kiasi cha kuingia mkataba na WCB Wasafi. Ni jambo la kheri.

Kitu kimoja ambacho ni muhimu sana kukikumbuka ni kwamba vita dhidi ya madawa ya kulevya sio ya mtu mmoja. Ni yetu sote. Ray C amewahi kuachana na matumizi. Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliingilia kati na kumsaidia. Ray C akawa Balozi wa kupiga vita matumizi ya madawa ya kulevya. She became vocal and for good reason. Akaanzisha mpaka NGO inayojishughulisha na vita hii nzito. Bila shaka alisaidia wengi wengine.

Nakumbuka hata ujumbe wake kwa Chid Benz pindi ilipojuliana wazi kwamba mwimbaji huyo wa Dar Stand Up alikuwa amefikia kubaya. Leo Chid Benz yupo “clean” na Ray C yupo rehab. Karudia tena. Wengi wanaacha na kisha kujikuta wamerudia tena. Tujiulize kwanini? Tunawapa support ya aina gani wakitoka? Kama jamii tunawaambia nini wanapotoka?

Kiufupi tuna wajibu wa kupiga vita biashara hii kutokea katika kiini chake (kwa wauzaji na wasambazaji). Kuwepo kwa madawa haya mitaani, ni chanzo cha kuendelea kwa matumizi. Yapo.Yanapatikana kirahisi. Wanaomuuzia Ray C na wengine,wapo. Hatuwajui? Ray C hamjui anayemuuzia? Hatujui wanapoyapata? Eeenh…polisi hamjui? Kwanini wananchi tunaishia tu kusema “fulani ni zungu la unga” na kutokwenda mbele kuwataja? Tunaishi nao mitaani. Hatuwajui? Hatuwaoni wakiingia na kutoka?

Serikali inajaribu. Jeshi la Polisi linaonekana kuwa na dhamira fulani katika vita hii. Ni jambo zuri. Ila serikali ilichukulie hili kwa mapana zaidi. Sio la Wizara Ya Mambo Ya Ndani tu. Wizara ya Elimu na Wizara Ya Afya ziungane pia. Utafiti unaonyesha wengi huanza matumizi ya madawa haya wakiwa mashuleni. Wazungu wa unga wanawanyemelea wakiwa mashuleni. Wanaweka kambi pembeni ya mashule. Tupanue vita huko pia. Wanafunzi waelimishwe kuhusu athari na jinsi ya KUSEMA HAPANA.

Vijana wengi wanajiingiza kwenye madawa ya kulevya kutokana na ukosefu wa shughuli maalum za kufanya. Wanakuwa wamekata tamaa. Wengi huanza kama kuonja ili kupunguza msongo wa mawazo (stress). Wengine ni tabia ya kuiga tu. Kitu ambacho hawajui ni kwamba madawa ni “addictive”. Ukianza huwezi kuacha kirahisi. Unakuwa “addicted”.Teja. Wanapomaliza rehab tunawapa muelekeo gani mpya? Tunawapa shughuli za kufanya? Kama ni La… si ni wazi kwamba baada ya muda mfupi tu wanarudia tena?

Chid Benz na Ray C(na hivi karibuni Fanani kutoka HBC) ni wanamuziki wenye majina makubwa. Wanafahamika. Ni rahisi kwao kusaidiwa hata kutokana na michango ya mashabiki zao. Huko mitaani wapo vijana wengi wanaoangamia. Hatuwajui kwa majina wala sura. Lakini ni watoto wa watu,kaka,dada,mjomba,baba,ndugu,rafiki wa wengine. Tuna wajibu. Wewe na mimi.

Ray C kila la kheri.

KIJANA SEMA HAPANA KWA MADAWA YA KULEVYA. FUATA NJIA HIZI.

 


Viewing all articles
Browse latest Browse all 180

Trending Articles